UATHIRIANOMATINI KATIKA USHAIRI WA KISWAHILI: MFANO WA UTENZI WA HATI NA UTENZI WA MWANAKUPONA
Abstract
Wataalamu wengi waliohakiki Utenzi wa Hati (1966) na Utenzi wa Mwanakupona (1860) wamedai kwamba UH umeathiriwa kwa kiasi kikubwa na Utenzi wa Mwanakupona (1860) katika fasihi ya Kiswahili bila kutoa ushahidi wa kina kiakademia. Wengi wao wamegusia tu kijuujuu kipengele cha kimaudhui bila kuongozwa na nadharia maalumu. Ni kama wamefumbia macho uketo wa utenzi huu na hivyo kukosa kuuangazia kwa nguvu sawa na UMK japo zina muundo na muono mmoja wa kimaudhui.Tenzi hizi kitarehe zimepishana kwa takriban zaidi ya miaka mia katika historia ya Pwani. Kulingana na Ruo, (1989) tenzi hizi zimekusudiwa kuadibu, kuasa au kutoa maoni juu ya maadili ya maisha. Katika UH sambamba na ilivyo katika UMK mshairi kwa ubunifu mkubwa anatoa mwongozo wa maisha kwa bintiye kama ulivyo wajibu wa mzazi yeyote kwa mwanawe. Sheikh Shaaban bin Robert kupitia UH anatoa wasia kufidia hali fulani iliomkumba katika maisha yake kumwelekeza mwanawe asijepotoka hali inayoshabihiana na ya Mwanakupona binti Mshamu katika UMK; Sheikh Shaaban bin Robert kufiwa na Amina, mkewe na kujitwika jukumu la mama kwa bintiye Mwanjaa kumfunza maisha na mambo ya unyumba; na Mwanakupona binti Mshamu naye kupatwa na maradhi kisha kuugua kwa muda wa mwaka asiweze kusema na mwanawe Mwanahashima kuweza kumuusia kuhusu maisha hasa maisha ya ndoa. Bakhtin (1981) mwasisi wa Usemezano haoni kama ushairi una usemezano au uathiriano na ushairi mwingine kwa kiwango sawa na riwaya. Haamini kuwa ushairi una umuhimu wowote katika mawanda ya Usemezano kwa kuwa uhai wake ulikwisha zamani. Kwa mtazamo wake, riwaya ndio utanzu unaotegemea zaidi uathiriano na matini nyingine wala si ushairi; ushairi matini yake imefungika, haibadiliki na haikubali uathiriano ndanimwe kama riwaya ambayo imefunguka na inanyumbuka kila leo. Utafiti huu umedhamiria kubadili mtazamo huu unaofungamanisha ushairi na uhafidhina wa maudhui, mfinyo wa mtindo na ndimi za usemi kujadili uathiriano wa matini za kishairi. Katika kuafikia azma hiyo, utafiti huu ulijikita katika malengo matatu: kubainisha maudhui ya UH yalivyoathiriwa na UMK, kuonyesha mtindo wa UH ulivyoathiriwa na UMK na kubainisha ndimi za usemi katika UH zilivyoathiriwa na UMK. Data ya kimsingi ilikusanywa maktabani kwa kuzingatia maudhui, mtindo na ndimi za usemi kwa mkabala wa kimaelezo, kusoma kazi teule, vitabu, majarida, tasnifu na katika mtandao. Data ya viambishi, maneno, mishororo na beti iliyopatikana ilichanganuliwa kwa kuzingatia malengo ya utafiti na nadharia ya Usemezano. Aidha, mifano iliyotolewa ilitoka katika UH na UMK kulingana na ufanifu wake. Utafiti huu ulibainisha uathirianomatini katika tenzi teule kwamba UH umesemezwa na UMK katika ushairi wa Kiswahili, hali ambayo kwa Bakhtin ni muhali kutokea. Uathiriano huu ulidhihirika katika maudhui, mtindo na ndimi za usemi. Utafiti huu unatoa mchango muhimu katika fasihi ya ushairi wa Kiswahili pamoja na kuirutubisha nadharia ya Usemezano kiuathirianomatini kwa kumulikia ushairi wa tenzi na ndimi za usemi ndanimwe kwa kuitononosha na usemi wa kidini ambao kwa mujibu wa Bakhtin ni wa kupewa, haukosoleki wala kuingiliana na ndimi nyingine. Pia, umetoa pendekezo la kuangalia upya mtazamo wa kuhakiki maudhui ya kifasihi hasa yaliyoruwazwa na mwonolimwengu wa dini ya Kiislamu bila kuyafinya katika “maudhui ya dini”