UCHANGANUZI WA TONOLOJIA YA KICHONYI KWA MKABALA WA NADHARIA YA FONOLOJIA VIPANDESAUTI HURU
Abstract
Toni katika lugha toni hudhihirika wakati wa uzungumzaji na hufanya neno kuwa na maana zaidi ya moja. Neno lenye toni linapotumika katika sentensi, mabadiliko ya toni huweza kuleta tofauti ya maana katika sentensi mahususi. Utafiti huu unahusu uchanganuzi wa toni inavyodhihirisha maana katika sentensi zenye nomino na vitenzi vya lugha ya Kichonyi kwa kudhihirisha michakato mahususi ya Tonolojia ambayo nomino na vitenzi hivyo hupitia na kanuni zinazodhibiti michakato hiyo.
Uchanganuzi huu unaongozwa na nadharia ya Fonolojia Vipandesauti Huru iliyoasisiwa na Goldsmith (1976). Msingi mkuu wa nadharia hii ni kuwa vipengele vya kifonolojia ni huru lakini vinahusiana katika usemaji wa lugha. Goldsmith (1976), alipendekeza kwamba vipengele hivyo viwakilishwe katika rusu wakati wa uchanganuzi. Yaani, kila kipengele kiwe na rusu yake ambayo ni; rusu ya vitamkwa, rusu ya viunzi, rusu ya viini toni, rusu ya toni na rusu ya usilabi.
Utafiti huu ulifanyika katika kaunti ndogo ya Chonyi, kauti ya Kilifi jimbo la Pwani. Utafiti wenyewe ulikuwa wa maktabani na nyanjani ambapo mbinu ya usampulishaji wa kimakusudi ilitumika katika kuteua maeneo ya utafiti yaliyohusishwa ambayo ni Ziani, Chasimba na Mwarakaya.
Data ya utafiti huu ni nomino na vitenzi vya Kichonyi vilivyokusanywa maktabani. Data hii ilitumiwa nyanjani ili kupata sentensi kamili zilizodhihirisha toni kutoka kwa wazungumzi wenyeji wa lugha ya Kichonyi. Data hii ilichunguzwa ili kuchanganua michakato mahususi ya Kitonolojia ambayo inahusika katika nomino na vitenzi vya Kichonyi hadi kuleta tofauti ya kileksia na kikategoria katika maneno yenye toni. Vilevile, kanuni zinazothibiti michakato hiyo zilibainishwa na kuwekwa wazi. Tasnifu hii imepangwa katika sura tano.
vi
Sura ya kwanza ni utangulizi ambapo mtafiti ameshughulikia usuli wa mada, suala la utafiti, madhumuni ya utafiti, maswali ya utafiti, upeo na mipaka ya utafiti, natija ya utafiti na changamoto za utafiti.
Katika sura ya pili mtafiti aliangazia mapitio ya maandishi ya tafiti zilizoshughulikia toni. Vilevile, tafiti zilizoshughulikia Kichonyi na lugha nyingine za Mijikenda zilifafanuliwa katika sura hii. Isitoshe, tafiti zilizochanganua michakato na kubainisha kanuni za toni ziliangaziwa hatimaye misingi ya nadharia na msingi wa kidhana inayoongoza utafiti ikaelezwa katika sura hii.
Sura ya tatu ya utafiti huu ilifafanua mbinu za utafiti zilizotumika ambapo mbinu ya uchunguzi shiriki ilitumika katika mazungumzo ya kawaida. Data ilikusanywa kwa kutumia majadiliano ya vikundi lengwa katika makundi teule ambapo data hiyo ilinakiliwa katika kitabu kwa kutumia kalamu. Vilevile, kinasasauti kilitumika katika kurekodi data ya utafiti huu kwa uchanganuzi zaidi.
Katika sura ya nne, mtafiti alishughulikia swala la uchanganuzi wa data ambapo data iliyokusanya ilichanganuliwa na toni katika nomino na vitenzi vya lugha ya Kichonyi ilitambulishwa. Aidha, michakato na kanuni zinazotawala nomino na vitenzi vya lugha ya Kichonyi ilichanganuliwa na kubainishwa. Sura ya tano ndiyo inahitimisha tasnifu hii na imeangazia muhtasari wa matokeo, hitimisho na mapendekezo. Utafiti huu una mchango mkubwa katika kukuza elimu ya isimu ya lugha za Kiafrika pamoja na kuendeleza elimu ya tonolojia katika lugha zenye toni.
Matokeo ya utafiti huu yatasaidia katika kuziba mwanya wa kiisimu katika lugha ya Kichonyi kwa kueleza kitaalamu tonolojia ya Kichonyi. Aidha, utafiti huu utasaidia katika kuendeleza matumizi ya nadharia ya Fonolojia Vipandesauti Huru.