UCHANGANUZI WA KIMOFOFONOLOJIA WA MANENO-MKOPO YA KIMBEERE KUTOKA LUGHA YA KISWAHILI
Abstract
Utafiti huu umechanganua kimofofonolojia maneno-mkopo ya lugha ya Kimbeere
kutoka lugha ya Kiswahili ili kutambua nomino- mkopo na vitenzi- mkopo vya asili ya
Kiswahili katika lugha ya Kimbeere. Malengo ya utafiti huu ni; kutambulisha nomino-
mkopo na vitenzi-mkopo vilivyotoka lugha ya Kiswahili na kuingizwa katika lugha ya
Kimbeere, kufafanua mifanyiko ya kimofofonolojia iliyohusika katika ukopaji wa
nomino-mkopo na vitenzi- mkopo vya Kiswahili na kuingizwa katika Kimbeere na
kubainisha kanuni za kiisimu zinazoongoza ukopaji wa nomino na vitenzi vya Kiswahili
katika lugha ya Kimbeere.Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Fonolojia Zalishi
Asilia (FZA) inayoangaziwa na Hooper (1976). Utafiti huu ni wa nyanjani na maeneo
ya utafiti yaliyoteuliwa ni Ishiara, Kanyuambora, Kamumu, Ugweri na Siakago. Data
ya kimsingi ya utafiti huu ilikuwa nomino-mkopo na vitenzi-mkopo vya lugha ya
Kimbeere vinavyotokana na lugha ya Kiswahili. Nomino na vitenzi hivyo vilitokana na
shughuli mbalimbali za maduka ya chakula, plastiki na mboga. Mbinu iliyotumika
katika ukusanyaji wa data ni Uchunguzi Shiriki. Mbinu hii ilimbidi mtafiti aende
nyanjani na kufanya kazi kama mhudumu madukani kwa muda wa wiki moja katika kila
duka. Katika ukusanyaji data wake, mtafiti alinakili nomino-mkopo na vitenzi-mkopo
kwenye daftari moja kwa moja kutoka kwa wazungumzaji waliofika madukani.
Kurekodi sauti za wazungumzaji pia kulihusika katika ukusanyaji wa data. Hii
ilimwezesha mtafiti kunasa matamshi mahsusi ya nomino-mkopo na vitenzi-mkopo
zilizokusanywa. Baada ya kukusanywa, data ilichanganuliwa kwa kuzingatia hatua
mahsusi. Kwanza mtafiti aliteua idadi ya watu kumi wenye umri wa kati ya miaka sitini
na sabini ambao ni wazawa na wanaojua lugha ya Kimbeere vizuri ili kubaini maneno
ya kukopwa na yasiyo ya kukopwa. Mtafiti kisha aliziweka nomino-mkopo na vitenzi-
mkopo katika makundi. Baadaye nomino-mkopo na vitenzi-mkopo hivyo viliweza
kunukuliwa kifonetiki. Mabadiliko ya sauti katika nomino-mkopo na vitenzi-mkopo
hivyo kisha yalitambuliwa na sauti mahsusi zilizobadilika kuweza kuthibitishwa.
Baadaye ruwaza za mabadiliko ya fonimu zilizotambuliwa na hatimaye kanuni
zinazotawala michakato mahsusi ya kimofofonolojia ziliwekwa bayana.Utafiti huu una
mchango mkubwa katika kuikuza lugha ya Kimbeere kwa sababu lugha hukua kadri
inavyofanyiwa utafiti. Utafiti huu pia unaendeleza taaluma ya isimu linganishi kwani
unahusu lugha ya Kiswahili na Kimbeere na mwingiliano wazo. Aidha, utafiti huu
unakuza elimu ya isimu ya lugha za Kiafrika pamoja na kuendeleza elimu ya upataji
lugha.