NJEO, HALI NA DHAMIRA KATIKA KITENZI CHA KITIKUU: MTAZAMO WA UMINIMALISTI
Abstract
Tasnifu hii inahusu uchanganuzi wa kiufafanuzi wa kimofosintaksia wa njeo, hali na
dhamira katika kitenzi cha Kitikuu. Njeo, hali na dhamira ni kategoria za kisarufi
zinazopatikana katika kitenzi. Kitikuu ni lahaja mojawapo kati ya lahaja za Kiswahili.
Kitenzi cha Kitikuu kina uwezo wa kubeba mofimu anuwai zenye uamilifu wa aina
mbalimbali. Kati ya mofimu zinazopatikana katika kitenzi cha Kitikuu ni mofimu za
njeo, hali na dhamira. Njeo ni kategoria ya kisarufi inayohusu uhusiano wa kiwakati wa
kutendeka kwa tendo hasa kwa kurejelea wakati wa sasa. Hali nayo huangalia jinsi
kitendo husika kinavyotendeka na wakati na kueleza kutimilika au kutotimilika kwa
kitendo hicho. Nayo dhamira huonyesha nia au lengo la msemaji kama ni kuarifu,
kuamuru, kusihi na kadhalika.
Madhumuni ya utafiti huu ni kuelezea na kuainisha njeo, hali na dhamira katika lahaja
ya Kitikuu na kuonyesha muingiliano wake katika lahaja hii. Nadharia ya Uminimalisti
imetumika kuonyesha jinsi ukaguzi wa sifa unavyofanya kazi kwa vipashio hivyo vya
njeo, hali na dhamira. Sentensi anuwai zenye kutumia mofimu hizo zimeonyeshwa na
mifano ya uchanganuzi ya baadhi za sentensi, kwa kutumia nadharia ya Uminimalisti.
Kulingana na Uminimalisti mofimu za njeo, hali na dhamira hupachikwa katika kitenzi
kupitia mchakato wa kimkokotoo. Leksika za vitenzi na nomino hupewa mofimu zao
katika leksikoni. Numerali huchagua sifa za kimofosintaksia za lugha fulani, baadaye
muungano hutokea kwa kuunganisha chembechembe mbalimbali za lugha na kuunda
maneno, virai na sentensi, hivyo kuunda miundo. Usogezi hutokea panapokuwa na
haja, kwani usogezi huchochewa na haja za kimofosintaksia. Kitikuu kwa sababu ni
lugha ambishi bainishi yenye ukwasi wa mofolojia, huruhusu usogezi ili kukagua sifa
za uzalishaji kuhakikisha ukubaliano na mahali pa kisintaksia katika sentensi. Mofimu
za njeo, hali na dhamira katika kitenzi cha Kitikuu hukaguliwa katika sehemu
vi
mbalimbali kuangazia ukubaliano wa kisarufi ili zisionekane katika umbo la kifonetiki
(UF).
Data juu ya njeo, hali na dhamira ilikusanywa kutoka maeneo ya Kizingitini, Tchundwa
na Rasini, kwa watu wasiopungua umri baina ya miaka 45 hadi 70. Mtafiti pia alitumia
umilisi wake alionao kuhusu lahaja hii ya Kitikuu, kama data msingi. Data ya ziada ni
ya kutoka maktabani, ambapo upekuzi wa maktabani ulifanywa kuhusu lahaja ya
Kitikuu, nadharia ya Uminimalisti na sarufi ya Kiswahili Sanifu.
Kitikuu kina njeo mbili kuu: njeo iliyopita {li} na njeo ijayo {ta}. Kitikuu, kwa nadra
hutumia njeo iliyopo {a} hasa katika vitenzi visaidizi. Kwa upande wa hali
imegawanywa katika hali timilifu na hali isiyo timilifu. Hali timilifu hutumia mofimu
{ndo} na {ie}. Hali isotimilifu hugawika katika hali mbalimbali kama hali ya mazoea
{hu}, hali ya mfululizo {ka} na hali ya kuendelea {hu} na {ki}. Kuna dhamira
mbalimbali zinazoonyeshwa kwa mofimu za kiishio {a} na {e} na dhamira za masharti
zikionyeshwa kwa mofimu {ki} na {ngali}.