UCHANGANUZI WA MAUDHUI YA SIASA KATIKA HADITHI MBILI, KIKAZA YA ROBERT ODUORI NA UTEUZI WA MOYONI YA RAYYA TIMAMMY
Abstract
Utafiti huu umeshughulikia uchanganuzi wa maudhui ya siasa jinsi yanavyodhihirika katika hadithi iliyotungwa na Oduori, Kikaza na hadithi iliyotungwa na Timammy, Uteuzi wa Moyoni. Mbali na kuchanganua maudhui, utafiti huu umechanganua mbinu za sanaa zilizotumiwa na watunzi Oduori na Timammy, katika kujenga maudhui ya siasa. Utafti huu uliongozwa na malengo matatu ambayo ni: kuchanganua maudhui ya siasa katika hadithi lengwa, kudhihirisha jinsi siasa zinavyoweza kuathiri maendeleo ya nchi na kuziweka bayana baadhi za mbinu za kisanaa zilizotumiwa na watunzi wa hadithi, Kikaza na Uteuzi wa Moyoni. Maswali yanayoongoza utafiti huu ni: Ni maudhui yapi ya siasa yanayojitokeza katika hadithi, Kikaza na hadithi, Uteuzi wa Moyoni? Ni jinsi gani siasa zinavyoathiri maendeleo ya jamii? Na ni mbinu zipi za kisanaa zilizotumiwa katika hadithi, Kikaza na Uteuzi wa Moyoni zilizowawezesha watunzi kuyasawiri maudhui ya siasa? Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Uhalisia iliyoasisiwa na Gustave Flaubert aliyeshikilia kuwa mtu hufikiria kwa kichwa chake hafikirii kwa moyo wake. Uhalisia ni nadaharia inayozingatia falsafa ya kiyakinifu; nadharia ambayo huwa na msisitizo mkubwa kwenye misingi ya hali za kiyakinifu za maisha kama vile mazingira ya kuishi, kuliko mawazo katika maisha ya binadamu. Utafiti huu ni wa maktabani. Data za msingi zilizoongoza utafitii huu zimekusanywa kutoka kwa hadithi ya Oduori, Kikaza na ile ya Timammy, Uteuzi wa Moyoni. Mtafiti amekusanya baadhi ya data za upili kutoka maktabani kwa kusoma kazi nyinginezo zinazohusiana na utafiti huu. Kazi hizo ni pamoja na: vitabu, majarida, makala, tasnifu, magazeti na hata kwenye mtandao. Data zilizokusanywa zilichanganuliwa kwa mbinu ya kimaelezo.Nazo mbinu za sanaa zilizodhihirika ni: jazanda, methali, misemo, nahau, kinaya, kejeli, tashtiti, tashihisi, majazi, hadithi ndani ya hadithi na nyenginezo.