UCHANGANUZI WA NOMINO-MKOPO ZA KIGIRYAMA KUTOKA KIINGEREZA
Abstract
Utafiti huu umechanganua kimofofonolojia nomino-mkopo za lugha ya Kigiryama
zinazotokana na lugha ya Kiingereza na kubainisha kanuni zinazoongoza michakato
mahsusi. Madhumuni ya utafiti huu ni kutambulisha nomino-mkopo zinazotoka katika
lugha ya Kiingereza hadi lugha ya Kigiryama katika shughuli za ukarabati na vifaa vya
magari, pikipiki na baisikeli, kudhihirisha michakato ya kimofofonolojia ambayo
inapitiwa na nomino-mkopo hizi na kubainisha kanuni za kimofofonolojia
zinazodhibiti ukopaji wa nomino kutoka lugha ya Kiingereza hadi lugha ya Kigiryama.
Nadharia ambayo iliongoza uchanganuzi huu ni Fonolojia Zalishi Asilia inayoangaziwa
na Hooper (1976).
Maeneo ya utafiti yaliyoteuliwa ni Bamba, Kaloleni, Kilifi, Malindi na Galana. Sampuli
ya magareji yaliyoteuliwa ni yale yanayopatikana karibu na miji ya maeneo mahsusi.
Data ya kimsingi ya utafiti ilikuwa nomino-mkopo za lugha ya Kigiryama
zinazotokana na lugha ya Kiingereza. Nomino hizi zinazotokana na vifaa na shughuli
mbalimbali za ukarabati zinazoendeshwa katika magereji ya magari, pikipiki na
baiskeli. Data ilikusanywa kwa kutumia mbinu ya Uchunguzi Ushirikishi ambapo
mtafiti alifanya kazi kama ‘spannerboy’ kwa muda wa wiki moja katika kila gereji
lililoteuliwa la makanika Wagiryama na kukusanya data ya nomino-mkopo za lugha ya
Kigiryama kupitia mazungumzo na mahojiano yao. Mtafiti alikusanya data kwa
kunakili nomino-mkopo moja kwa moja kutoka kwa wazungumzi wenyeji wa lugha ya
Kigiryama . Ukusanyaji data pia ulihusisha kurekodi sauti za wazungumzaji ili kuweza
kunasa matamshi mahsusi ya nomino-mkopo zilizokusanywa.
Data ilichanganuliwa kwa kuzingatia hatua mahsusi. Kwanza nomino-mkopo
zilipangwa katika makundi na kunukuliwa kifonetiki. Kisha mabadiliko ya sauti katika
v
nomino-mkopo hizi yalitambuliwa na sauti mahsusi zinazobadilika kuweza
kuthibitishwa. Baadaye ruwaza za mabadiliko ya fonimu zilitambuliwa na hatimaye
kanuni zinazotawala michakato mahsusi ya kimofofonolojia ziliweza kuwekwa bayana.
Maelezo, ufafanuzi, michoro na majedwali yalitumiwa katika utafiti huu.
Tasnifu hii imepagwa katika sura tano. Sura ya kwanza inashughulikia utangulizi wa
utafiti kwa kuzingatia misingi ya utafiti huu na kuweka bayana swala la utafiti,
madhumuni ya utafiti, nadharia tete, upeo wa utafiti na natija ya utafiti. Katika sura ya
pili, misingi ya nadharia ya utafiti huu pamoja na misingi ya kidhana imewekwa
bayana. Sura ya tatu inaeleza utaratibu wa utafiti, eneo la utafiti, jumuia na uteuzi wa
sampuli, vifaa vya kukusanyia data, utaratibu wa kukusanya data, jinsi data
ilivyochanganuliwa, pamoja na kuonyesha uaminiki na maadili yaliyozingatiwa katika
utafiti huu.
Sura ya nne inashughulikia uchanganuzi wa data na matokeo ya utafiti na sura ya tano
inatamatisha utafiti huu kwa kutoa hitimisho la utafiti huu na mapendekezo ya mada
zingine zinazoweza kufanyiwa utafiti.
Utafiti huu ni mchango muhim katika taaluma ya isimu linganishi kwa jinsi ambavyo
unahusisha lugha mbili – Kiingereza na Kigiryama. Zaidi ya hayo, utafiti huu unasaidia
katika ufundishaji wa lugha ya pili kwa sababu vikwazo vya kifonolojia vya lugha hizi
mbili vimewekwa bayana. Kwa jumla utafiti huu unachangia katika kuweka hai na
kuendeleza lugha ya Kigiryama kwa sababu imeweza kupata ukwasi wa istilahi za
kuweza kutumika katika uwanja wa kiteknolojia wa ukarabati wa magari, pikipiki na
baiskeli. Kwa jumla utafiti huu ni mchango mpya katika tafiti za kiisimu za lugha ya
Kigiryama na pia ni hazina kubwa katika uwanja wa Isimu za lugha za Kiafrika.