MITAZAMO YA WAANDISHI WA KIKE NA WA KIUME KUHUSU USAWIRI WA WAHUSIKA WA KIKE KATIKA TAMTHILIA ZA KISWAHILI
Abstract
Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa ni kuchunguza mitazamo ya waandishi wa kike na
wa kiume kuhusu usawiri wa wahusika wa kike katika tamthilia za Kiswahili. Mtafiti
aliongozwa na malengo matatu. Kwanza, ni kutambulisha jinsi waandishi wa kike
walivyowasawiri wahusika wa kike katika tamthilia zilizoteuliwa. Pili, kuonyesha jinsi
waandishi wa kiume walivyowasawiri wahusika wa kike katika tamthilia
zilizoteuliwa.Mwisho, ni kulinganisha na kubainisha mitazamo ya waandishi hao kama
walivyowasawiri wahusika wa kike. Sifa mbalimbali waandishi hao walizowapa
wahusika wa kike katika tamthilia zao, zimeonyesha tofauti za kimitazamo baina yao.
Aidha, utafiti huu umeonyesha waandishi walio na mitazamo chanya na vilevile walio
na mitazamo hasi kwa wahusika wa kike.
Matokeo ya utafiti huu yameonyesha kuwa waandishi wa kike huwasawiri wahusika wa
kike kwa mtazamo hasi katika tamthilia za Kiswahili. Pia, umeonyesha baaadhi ya
sababu ambazo yamkini ndizo zilizowachochea baadhi ya waandishi kuwa na mitazamo
tofauti kuhusu wahusika wa kike kwenye kazi zao za kifasihi.
Utafiti uliongozwa na nadharia ya Ufeministi wa Baada-ukoloni inayohusishwa Said
(1993) na baadaye kutiwa nguvu na Mills (1995). Nadharia hii inasaili jinsi mataifa ya
kimagharibi yalivyousawiri utamaduni wa nchi za Kiafrika. Nadharia hii inadai kuwa
mtagusano wa kitamaduni baina ya mataifa tawala na mataifa tawaliwa ulisababisha
athari kuhusu mahusiano ya kijinsia barani Afrika. Kwa hivyo, usawiri wa wahusika wa
kike katika mataifa ya ulimwengu wa tatu ni mwigo wa mitazamo ya wakoloni
waliotawala barani Afrika kabla ya uhuru.
Tasnifu hii imegawanywa katika sura tano. Sura ya kwanza imeshughulikia usuli wa
mada, madhumuni ya utafiti, maswali ya utafiti, upeo, natija ya utafiti na maelezo ya
vi
istilahi. Sura ya pili inajumuisha mapitio ya maandiko na msingi wa nadharia. Sura ya
tatu, inahusu mbinu za utafiti na ukusanyaji wa data, utaratibu wa utafiti, jumuiya na
uteuzi wa sampuli. Aidha, inahusu mbinu za ukusanyaji data, vifaa vya kukusanyia data,
uchanganuzi wa data, maadili ya utafiti, uaminikaji na utegemewaji wa utafiti na msingi
wa kidhana. Sura ya nne imegawanyika katika sehemu tatu. Kwanza, ni mitazamo ya
waandishi wa kike. Pili, ni mitazamo ya waandishi wa kiume na tatu, ulinganishaji wa
mitazamo ya waandishi kijinsia. Sura ya tano ni hitimisho, sababu za usawiri na
mapendekezo.
Utafiti huu umefanywa maktabani. Mbinu zilizotumiwa ni; upekuzi wa makala na matini
mbalimbali, usomaji wa tamthilia zilizohusika, kunakili na kuorodhesha sifa za
wahusika wa kike. Aidha, michoro, chati, majedwali na tarakimu zilitumiwa
kuwakilisha hali mbalimbali.
Utafiti huu utawanufaisha wasomaji na wahakiki wa kazi za kifasihi. Kwanza,
umebainisha mitazamo tofauti ya waandishi wa tamthilia za Kiswahili. Umeonyesha
kuwa waandishi wa kike wanawasawiri wahusika wa kike kwa mtazamo hasi zaidi
wakilinganishwa na waandishi wa kiume. Halikadhalika, umekuwa tathmini ya juhudi
za waandishi wa tamthilia za Kiswahili katika kuibadilisha taswira ya mwanamke katika
fasihi na jamii. Pia, ni mchango katika mdahalo wa mahusiano ya kinjisia unaoendelea
kote ulimwenguni.
Mtafiti amehakiki tamthilia nne. Mbili za waandishi wa kike ambao ni Katini Mwachofi;
Mama Ee na Catherine Kisovi aliyeandika Dunia Hadaa. Waandishi wa kiume ni
Alamin Mazrui na Kimani Njogu ambao wameandika