USAWIRI WA MWANAMUME KATIKA METHALI ZA KIMERU NCHINI KENYA
Abstract
Utafiti huu unahusu uchanganuzi wa usawiri wa mwanamume katika methali za
Kimeru. Imebainika kuwa usawiri wa mwanamume katika methali za Kimeru
haujawekwa bayana na utafiti wowote. Utafiti huu umebainisha jinsi mwanamume
alivyochorwa kitaswira kupitia methali. Jamii ya Wameru ni ya kabila la Kibantu
ambalo linaegemea mno upande wa kuumeni. Hivyo, kuna methali nyingi
zinazomtaja mwanamume.
Nyanja nne kuu za hali za kawaida za maisha katika jamii ya Wameru
zimechunguzwa ili kufanikisha utafiti huu. Nyanja hizo ni pamoja na tohara, ndoa,
kazi na utawala. Hali hizi nimezichaguwa hususan kwa sababu ndizo nguzo kuu za
maisha ya binadamu katika mtazamo wa jamii hii.
Utafiti huu uliongozwa na nadharia za ubabeume na uamilifu wa kimuundo. Nadharia
tete za utafiti huu ni: methali zinampa mwanamume hadhi ya juu na pia hudhihirisha
nafasi na majukumu ya mwanamume katika jamii.
Mbinu mbili kuu na muhimu za kukusanyia data zilitumika, nazo ni: mahojiano na
udadisi. Jumla ya methali thelathini zilikusanywa, kufasiriwa na kuchanganuliwa
kithamano. Ilibainika kuwa mwanamume alipewa majukumu ya kipekee kupitia
methali. Matokeo yalipobainika mapendekezo mwafaka yalitolewa.