UCHANGANUZI WA MAUDHUI YA NYIMBO ZA MSONDO NA ATHARI ZAKE KWA WANANDOA KATIKA JAMII YA WADIGO
Abstract
Nyimbo za msondo za jamii ya Wadigo ni aina za nyimbo ambazo huimbwa wakati wa harusi upande wa kwa bi. harusi na huwa tofauti kabisa na nyimbo za harusi za kawaida. Utafiti huu ulinuia kuchanganua maudhui ya nyimbo za msondo na athari zake kwa wanandoa katika jamii ya Wadigo. Malengo matatu yaliongoza utafiti huu yakiwemo kuchanganua maudhui yanayojitokeza katika nyimbo hizi za msondo, kubainisha miiko inayofungamanishwa na nyimbo hizi na kubainisha athari zinazohusishwa na nyimbo hizi za msondo. Ili kutimiza malengo haya mtafiti aliongozwa na nadharia ya uhalisia kwani maudhui ya nyimbo za msondo na athari zake zinahusishwa na utamaduni wa mila ya jamii ya Wadigo ambayo hufungamana na maisha yao ya kila siku. Nadharia hii ilitumika katika utafiti huu kwa sababu inashikilia kwamba hali zote za maisha ya kijamii hustahili kuelezwa katika uhalisi wake kama unavyoonekana wala sivyo unavyofikiriwa kuwa. Utafiti huu ni wa kithamano huku ukizingatia muundo wa kimaelezo. Mbinu za uchunguzi shirikishi katika miktadha isiyo rasmi na mahojiano zilitumika katika ukusanyaji wa data. Data zilikusanywa kutoka nyanjani ambapo mtafiti alionana ana kwa ana na watafitiwa. Sampuli ya kimaksudi ilitumika kuteua mshiriki mmoja ambaye alisaidia katika uteuzi wa washiriki wengine kupitia sampuli tajwa. Sampuli hii ili jumlisha watu hamsini wakiwemo makungwi, wanawake waliochezewa nyimbo za msondo, wanawake ambao hawakuchezewa nyimbo za msondo na wanaume waliopo katika ndoa ili kutoa maoni yao kuhusiana na mafunzo ya nyimbo hizi. Data hii ilichanganuliwa na kuwasilishwa kutumia grafu ambapo asilimia ya watafitiwa ndio iliyotumika kuelezea maoni ya wanajamii kuhusiana na mada hii ya utafiti. Utafiti huu utatoa mchango wa kueleza utamaduni, mila na desturi za jamii ya Wadigo na kuweka wazi masuala ya nyimbo hizi za msondo kiakademia. Utafiti huu vilevile utachangia katika hazina ya maswala ya fasihi simulizi ya Afrika.
vi
YALIYOMO