UCHANGANUZI WA ATHARI ZA KIMOFOFONOLOJIA MIONGONI MWA WANAFUNZI WA KISOMALI WANAPOJIFUNZA LUGHA YA KISWAHILI
Abstract
Utafiti huu ulishughulikia makosa ya kimofofonolojia miongoni mwa wanafunzi wa Kisomali wanapojifunza Kiswahili sanifu kama lugha yao ya pili. Utafiti huu ulifanywa katika shule za upili za umma katika kaunti–ndogo ya Garissa-Township, Garissa kaunti, nchini Kenya. Lugha ya Kisomali imefanyiwa utafiti katika vipengele mbalimbali katika maeneo tofautitofauti lakini hakuna utafiti ambao umewahi kufanywa katika maeneo ya Garissa. Basi utafiti huu ulilenga kuziba mwanya huu wa kielimu hasa katika kiwango cha kimofofonolojia katika lugha ya Kisomali, eneo la Garissa.
Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Uchanganuzi Makosa (N.U.M) ambayo iliasisiwa na Corder mwaka wa 1967, ambaye anasema kuwa kufanya kosa ni njia mojawapo ya kujifundisha lugha ya pili. Kwa hivyo, mwanafunzi anapofanya kosa, asiadhibiwe bali chanzo cha kosa kibainishwe.
Data iliyohusishwa ilitoka nyanjani na ilikuwa makosa ya kimofofonolojia katika lugha ya Kiswahili yanayofanywa na wanafunzi wenye asili ya lugha ya Kisomali kutoka shule za upili za umma za kaunti-ndogo ya Garissa-Township. Data ya nyanjani ilikusanywa kwa kutumia mbinu ya kuandika insha na kusimulia hadithi ambapo wanafunzi wa kidato cha tatu waliokuwa wameteuliwa waliandika insha na kusimulia hadithi. Wanafunzi hawa waliteuliwa kwa sababu walikisiwa kuwa wamepata umilisi wa lugha ya Kiswahili na hawakuwa katika pilka pilka za kujiandaa kwa mtihani wa kitaifa. Mtafiti alikusanya insha ili kuzisoma na kanda alizokuwa amerekodi ili kuzisikiliza na kutambua makosa ya kimofofonolojia yaliyofanywa na wanafunzi. Hii ndio ilikuwa data ya utafiti.
Data ilichanganuliwa kwa kutumia uchanganuzi wa maelezo. Vifaa tulivyotumiwa ni insha na hadithi.