UCHANGANUZI WA MAKOSA YA KIMOFOFONOLOJIA KATIKA LUGHA YA KISWAHILI MIONGONI MWA WANAFUNZI WENYE ASILI YA LUGHA YA KIKAMBA
Abstract
Utafiti huu umechanganua makosa ya kimofofonolojia yanayofanywa na wanafunzi wa
shule za upili ambao ni wazungumzaji wa lugha ya Kikamba wanapojifunza lugha ya
Kiswahili kama lugha ya pili. Utafiti huu ulinuia kutambua makosa, kupata vyanzo vya
makosa hayo na kupendekeza njia za kuyatatua.
Utafitiuliongozwa na nadharia ya Uchanganuzi Makosa kama ilivyoasisiwa na Corder
(1960). Uchanganuzi Makosa ni mtazamo ambao hutumiwa kueleza makosa
yanayopatikana katika kazi za wanafunzi kwa kutambua makosa, kuyaainisha, kuonyesha
visababisho vya makosapamoja na kupendekeza njia za kukabiliana nayo.
Data ilikusanywa kutoka kaunti ya Makueni wilaya ya Nzaui. Aidha utafiti ulihusisha
shule nne kutoka wilaya ya Nzaui kaunti ya Makueni. Sampuli ya utafiti ilihusisha
wanafunzi wa kidato cha pili na cha tatu waliochaguliwa kushiriki katika utafiti.
Data ilichanganuliwa kwa kutumia nadharia ya uchanganuzi makosa ya Corder (1960).
Matokeo ya utafiti huuni kuwepo kwa makosa ya kimofofonolojia ya uchopekaji,
udondoshaji na matumizi ya sauti mbadala miongoni mwa wanafunzi wakamba
wanaojifunza lugha ya Kiswahili.