USHAHIDI UNAODHIHIRISHA KUWA KISWAHILI SI KIARABU
Abstract
Utafiti huu umeonyesha kuwa Kiswahili ni lugha kamili, huru inayoweza kujisimamia kama lugha nyingine yoyote. Vilevile umepinga swala la kuwa Kiswahili ni Kiarabu. Maneno asili ya Kiarabu yamefanyiwa utafiti kwa njia ya mahojiano, kujaza hojali na kuzuru madrasa mbalimbali ili kuzalisha visawe vya maneno asili ya Kiswahili kama vile neno ‘lawama’ lenye asili ya Kiarabu kupata kisawe chake katika lugha asili ya Kiswahili ambacho ni neno ‘matayo’. Wataalamu kama vile Mazrui na Sharif (1994) wanachukulia kuwa Kiswahili ni Pijini ya Kiarabu na lugha za Kibantu. Stigand (1915) na Reusch (1953) wanadai kuwa Kiswahili ni mojawapo kati ya lahaja za Kiarabu. Utata huu wa kihistoria wa kila mwanaisimu kusema hoja tofauti na mwingine ndio uliompelekea mtafiti kufanya utafiti huu wa kiisimu kwa lengo la kuziba pengo la upungufu wa data za kiisimu. Katika utafiti pengo la kiisimu limezibwa kwa njia ya kuorodhesha visawe vya kiasili (Kiswahili) – maneno yaliyopelekea kusemwa kuwa Kiswahili ni Kiarabu. Wajuzi wenye umri wa makamo wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu, wanaume na wanawake wapatao ishirini walihojiwa, walijaza hojaji na wengine, baadhi, walijadiliana na mtafiti kuhusu kupata maneno asili ya Kiswahili na Kiarabu. Madrasa mbili zilizoko Lamu zilitembelewa na walimu wa huko kuhojiwa na wengine wakajaza hojaji ambazo zilisaidia kuongeza data za kiisimu. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Umuundo iliyoasisiwa na Ferdinand de Saussure (1857-1913) inayohusisha uchunguzi na uchanganuzi wa viambajengo. Malengo ya utafiti huu ni Kuorodhesha visawe vya maneno ya kiasili ya Kiswahili vinavyoonyesha maana sawa na maneno ya Kiswahili yenye etimolojia ya Kiarabu, kuangalia tofauti zinazopatikana katika baadhi ya vipengele vya kisarufi kama vile hali ya umoja na wingi, unominishaji na uambishi katika maneno ya lugha hizi mbili zinazotafitiwa na mwisho ni kubainisha tofauti za maumbo na miundo katika maneno ya Kiswahili na Kiarabu. Maeneo ya utafiti yaliyotembelewa ni Mombasa, Amu, Siu, Pate na Matondoni. Haya ni maeneo ambayo kulingana na tafiti za historia ya Kiswahili ndiyo yenye Waswahili asili. Katika kipengele cha uchanganuzi wa data, maneno asili ya Kiswahili na Kiarabu yamedenguliwa kiisimu. Matokeo yake yamedhihirisha kuwa sarufi ya Kiswahili iko tofauti na sarufi ya Kiarabu kwa asilimia takriban 90%. Utafiti vilevile umebaini tofauti za kisemantiki na za kifonetiki zinazopatikana katika maneno mkopo ya Kiswahili kutoka lugha ya Kiarabu. Hapa, utafiti umeonyesha kuwa asilimia kubwa ya maneno mkopo kutoka lugha ya Kiarabu yanapoingizwa katika Kiswahili, mara nyingi maana asili hupotezwa na kubadilishwa au kubandikizwa maana mpya ili kutosheleza matumizi ya kiswahili. Kwa kuwa utafiti huu ulifanyika katika maeneo ya Lamu na viunga vyake na kulingana na historia ya chimbuko la Kiswahili yasema kuwa kitovu cha lugha hii ya Kiswahili ni Shungwaya, mtafiti apendekeza kuweko watafiti watakaofanya mada sawa na mada hii ya utafiti huu utakaofanywa huko Shungwa na maeneo ya Tanzania ili kupatikane ushahidi wa kina zaidi.
