MNYAMBULIKO WA VITENZI KATIKA LUGHA YA KIDIGO: MKABALA WA FONOLOJIA ZALISHI ASILIA
Abstract
Utafiti huu ulihusu mnyambuliko wa vitenzi katika lugha ya Kidigo kwa madhumuni ya
kubainisha kanuni zinaohusika katika mchakato wa kunyambua vitenzi katika lugha hii.
Kama lugha mojawapo ya Kibantu, lugha ya Kidigo ni miongoni mwa lugha ambayo
haijatafitiwa kwa upana hasa katika maswala ya kiisimu. Mnyambuliko wa vitenzi
umefanywa katika lugha mbalimbali za Kibantu ikiwemo Kigiriama, Kikuria,
Kirunyankole na kadhalika lakini haujafanywa katika lugha ya Kidigo. Utafiti huu hivyo
unanuia kuziba pengo hili. Malengo ya utafiti huu ni kubainisha mofimu za unyambuaji
katika vitenzi vya Kidigo kwa kutumia kauli mbalimbali, kuchambua mifanyiko ya
kimofofonolojia katika vitenzi vilivyonyambuliwa na kueleza kanuni za kimofofonolojia
zinazodhibiti mnyambuliko wa vitenzi vyenye asili ya lugha ya Kidigo. Umuhimu wa
utafiti huu ni kupambanua lugha ya Kidigo kwa misingi ya kiisimu ili kuweka misingi
thabiti ya sarufi ya lugha hii na vilevile kuongeza idadi ya tafiti zilizofanywa katika lugha
ya Kidigo. Data ya utafiti huu ni vitenzi vyenye asili ya Kidigo na vilikusanywa kutoka
nyanjani. Vitenzi vilikusanywa eneo la Msambweni katika kaunti ya Kwale kwa njia ya
mahojiano ambapo mtafiti alishiriki katika kuuliza maswali ili apate data yake. Data hii
baadae ilipangwa na kuchanganuliwa kwa misingi ya Nadharia ya Fonolojia Zalishi Asilia
ili kubainisha sheria zilizohusika na mnyambuliko wa vitenzi katika lugha ya Kidigo.
Mifanyiko ya kimofofonolojia iliyodhihirika baada ya kunyambua vitenzi vya Kidigo ni
sita nayo ni: uwiano wa irabu, uchopekaji, udondoshaji, ubadala wa fonimu, kuimarika na
kudhoofika kwa fonimu. Uchanganizi huu ulifanywa kwa njia ya maelezo yakisaidiwa na
michoro pamoja na majedwali. Matokea ya utafiti yalionyesha kuwa lugha ya Kidigo ni
lugha nyambulishi kwa jinsi ambavyo vitenzi viliweza kunyambulika katika kauli
mbalimbali. Utafiti pia uliweza kudhihirisha kuwa shughuli ya mnyambuliko wa vitenzi
katika lugha ya Kidigo huhusisha mifanyiko mbalimbali ya kimofofonolojia
inayoongozwa na sheria maalum